Hivi ulishawai kujiuliza kilitokea nini kwa nyota kama Mohammed Salah, Kevin De Bruyne, na Romelu Lukaku ndani ya Chelsea? kwanini walishindwa kung'aa ndani ya klabu hiyo?
Mohammed Salah alisajiliwa na Chelsea akitokea klabu ya FC Basel mara baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na klabu hiyo, lakini aliposajiliwa na klabu hiyo ya London hakufanikiwa kufanya vizuri, hiyo ilikuwa kipindi Chelsea ikiwa chini ya Jose Mourinho. Baadae nyota huyo alipelekwa kwa mkopo Fiorentina kabla ya baadae kuuzwa kwenda AS Roma tena kwa dau rahisi kabisa, aliuzwa kwa paundi milioni 11.
Leo hii Mohammed Salah anafanya vizuri klabuni Liverpool aliposajiliwa akitokea AS Roma, na kwa sasa ndiye nyota anayeongoza kwa ufungaji wa magoli katika ligi kuu Uingereza.
Hilo pia likatokea kwa mbelgiji, Kevin De Bruyne ambapo naye hakucheza kwa mafanikio Chelsea ingawa pia hakupata muda mwingi wa kuonyesha kipaji chake akitumia muda mwingi kukaa benchi lakini baadae alipouzwa kwenda Wolfburg ya Ujerumani katika msimu wake wa kwanza akaibuka kama mkali wa kutoa pasi za mwisho katika ligi kuu Ujerumani maarufu kama Bundesliga.
Leo hii, ukitaka kuwataja nyota 10 mpaka sasa katika ligi kuu Uingereza, huwezi kumuacha kumtaja nyota huyu ambaye anaiongoza vyema klabu ya Manchester city iliyo kileleni katika ligi kuu Uingereza.
Lakini nyota mwengine kutoka Ubelgiji ni Romelu Lukaku, aliwai kuhojiwa anadhani kwanini aliondoka Chelsea, jibu alilolijibu alisema "nadhani kutokana na kukosa penati (vs Bayern Munich katika mchezo wa Uefa Super Cup)".
Romelu Lukaku amekuwa moto wa kuotea mbali kwa sasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufunga tena akiwa na umri mdogo kabisa, miaka 24.
Hakucheza Chelsea kwa mafanikio kabla ya kupelekwa Everton aliyoichezea kwa mkopo kabla ya kuuzwa kabisa na baadae kutimkia Manchester united.
Sasa hao ni baadhi ya walioondoka Chelsea wakiwa bado timu inawahitaji, lakini ulishajiulizaga kwanini haswa hili linatokea kwa Chelsea?
Ross Barkley wa Everton alifika Chelsea ili kufanyiwa vipimo vya afya ili ajiunge na klabu hiyo lakini katikati ya vipimo alighairi na kuondoka kurudi Everton, unaelewa ni kipi kilimsibu?
Alex-oxlade Chamberlain alikaribia kutua Chelsea lakini mwishowe akatimkia Liverpool, kuna nini ndani ya Chelsea?
Virgil van Dijk baada ya Southampton kugoma kumuuza kwenda Liverpool walikuwa tayari kumuuza mlinzi huyo kwenda Chelsea, lakini mwenyewe aligoma na akalazimisha kwenda Liverpool kwanini?
Majibu haya yote nitakuletea katika sehemu ya pili ya makala haya...

Post a Comment
Post a Comment