WATATOKEA wapi kwa mfano? Ndilo swali linaloulizwa na kila upande Simba na Yanga, kuhusu mechi ya miamba hiyo ya soka leo, kila mmoja akihoji mwenzie atatokea wapi kukwepa kipigo katika mechi hiyo ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu bara.
Mechi hii pia unaweza kuiita ya kisasi na hasira. Simba ikitaka kulipa kisasi cha kufungwa mechi zote mbili msimu uliopita na Yanga ikitaka kumaliza hasira za kupoteza mechi yake iliyopita dhidi ya Stand United, hapo ndipo kila upande unapouliza mwenzake atatokea wapi.
Mara zote timu hizi zinapokaribia kukutana kunakuwa na presha kwa mashabiki, vituko, tambo na maandalizi ya kila aina. Mechi ya leo, ni tofauti na mechi mbili za msimu uliopita, ambapo Simba ilikuwa ikionekana dhaifu kukutana na Yanga iliyokuwa kamili kila idara.
Leo Simba inakutana na Yanga ikiwa kwenye mstari, inaongoza msimamo wa ligi kwa pointi 16 na ikiwa imeshinda mechi tano huku moja ikitoka sare. Simba ilishinda mabao 3-1 dhidi ya Ndanda, 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, 1-0 dhidi ya Azam FC na 4-0 dhidi ya Majimaji huku ikitoka sare ya bila kufungana na JKT Ruvu.
Lakini kwa upande wa Yanga, ipo vilevile kama ilivyokuwa msimu uliopita, washambuliaji wake wenye uchu wa kuzifumania nyavu kama walivyofanya msimu uliopita. Tofauti tu ni kwamba Yanga leo inakutana na Simba ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza moja katika mechi tano ilizocheza. Ina pointi 10.
Hata hivyo, Yanga bado ipo vizuri na wachezaji wake kuonekana kwenye kiwango cha juu na wazoefu zaidi wa mechi ngumu kutokana na ushiriki wao wa michuano ya kimataifa, tofauti na Simba ambao wana mwaka wa nne wachezaji wake hawajacheza michuano ya kimataifa na timu yao.
Yanga ilishinda dhidi ya African Lyon mabao 3-0, Majimaji 3-0, na Mwadui 2-0 na kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Ndanda FC huku ikifungwa bao 1-0 na Stand United.
Wauaji wa Yanga katika mechi dhidi ya Simba msimu uliopita bado wapo kwenye timu hiyo na wana nafasi kubwa ya kupata tena mabao. Hao ni Malimi Busungu, Amis Tambwe na Donald Ngoma waliohusika katika mechi ya kwanza na ya pili. Timu zote zimefanya maandalizi katika kambi kwenye maeneo tofauti kujiandaa na mchezo huo.
Yanga iliweka kambi yake Pemba, sehemu ambayo inaamini ina bahati nayo kwani inapoweka kambi huko hushinda mechi yake na Simba. Kwa upande wa Simba ilijichimbia Morogoro. Kila timu inajivunia kikosi bora msimu huu.
Simba ikiwa imebadilika kwa kiasi kikubwa huku washambuliaji wake Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya wakionekana kuibeba timu hiyo kwa kufunga mabao karibu katika kila mechi. Yanga bado ina wachezaji wale wale, Tambwe, na Msuva huku ikiwaongeza Juma Mahadhi ambaye kama atachezeshwa leo anaweza kuwa na madhara upande wa pili.
Yanga na Simba, zimekuwa zikitumia mfumo wa 4-4-2 ingawa mara moja moja hubadilika kutokana na mazingira ya mechi husika.
Kwa upande wa makocha, Joseph Omog wa Simba atakutana na Yanga kwa mara ya kwanza tangu kujiunga na timu hiyo akitokea Azam, lakini kocha wa Yanga, Hans van Pluijm anataka kutengeneza rekodi nyingine baada ya msimu uliopita kufanya vizuri kwa kuifunga Simba.
Post a Comment
Post a Comment