KWA miaka na miaka klabu mbili za soka kubwa na kongwe nchini, Simba na Yanga zimekuwa na ushindani wa jadi ambao ni wa enzi na enzi.
Simba na Yanga zote zina maskani yake jijini Dar es Salaam mitaa ya Kariakoo, Yanga ikiwa kwenye kona ya mtaa wa Twiga na Jangwani na Simba Msimbazi. Zimecheza mapambano mengi kati yao ambayo yamekuwa na historia lukuki ambazo hata kijana mdogo kabisa wa miaka ya karibuni anazijua kwa aidha kusoma mahali au kusimuliwa na wakubwa zake.
Kumekuwa na nyakati au vipindi vya mpito wa ‘utawala’ kati yao kwa miaka dahali sasa, ambapo kuna wakati timu mojawapo inaonekana kutawala kwa kumfunga mara nyingi au mfululizo mmoja wao. Lakini pia katika tawala hizi tofauti pia kuna wakati timu moja hutwaa vikombe vya ubingwa mfululizo huku mwingine akiwa msindikizaji. Hali hii imepelekea timu moja wapo kukosa kushiriki michuano ya kimataifa.
Imefikia takribani misimu minne sasa tangu Simba kwa mara ya mwisho ichukue ubingwa wa Tanzania Bara na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kimataifa. Sio ubingwa tu, bali hata nafasi ya pili ambapo kabla ya ujio wa kombe le Shirikisho –Azam Sports Federation Cup, ilikuwa unapata nafasi ya kushiriki pia kombe la Shirikisho la Soka Afrika – CAF.
Hali hii imefanya kupeana majina yasiyo rasmi ambapo mmoja hujiita Wakimataifa kwa ushiriki wake wa michuano ya kimataifa huku wakiwaita wenzao (Simba) wakiwaita wenzao Wamatopeni, wa mchangani kwa kukosa kwao kushiriki michuano ya kimataifa. Dumu daima lililo kuu kati yao ni nani anamfunga mwenzie katika mechi zao wanapokutana bila kujali yuko kwenye hali gani kwa maana ya nafasi ya kutwaa ubingwa au hapana.
Kuna nyakati au mpaka sasa inapofika wakati wa uchaguzi kwenye klabu hizi viongozi hupimwa kwa mara ngapi waliwafunga watani zao. Wagombea hutumia pia udhaifu wa timu yao kufungwa mara nyingi na mtani kama hoja ya kuombea kura kwa kusema akichaguliwa yeye basi atafuta unyonge wa kufungwa na mtani wake. Ukiangalia msimu uliopita, Yanga waliifunga Simba bao 2-0 kwenye mechi zote mbili, yaani kila mechi 2-0.
Mwisho wa msimu, Yanga ikatawazwa mabingwa huku Azam FC ikiwa washindi wa pili ambapo hata kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho ilikuwa ni Yanga na Azam zilizocheza na Yanga kutwaa kikombe. Siku zote inapotokea Simba au Yanga ikatwaa kikombe huku ikimfunga mtani inakuwa fu- raha iliyoje. Hii haiji tu kama watu wa- navyofikiria ila mara nyingi kama sio zote huendana na maandalizi ya kitaalamu.
Yanga haikubahatisha kuifunga Simba mara mbili msimu uliopita, bali ilifanya hivyo kwa kuwa uwezo wao uko juu kulinganisha na Simba. Ni dhahiri kwamba kwa sasa sio tu hapa Tanzania bali hata ukanda huu wa Afrika Mashariki Yanga wana kikosi kizuri chenye muunganiko mzuri pia.
Imewachukua Yanga sio chini ya miaka mitatu kukijenga kikosi chao ambacho wanacho sasa na matokeo yake tuliona wakifanikiwa kufika raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na kuingia kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho ambako hawakufanya vizuri sana. Wana kikosi imara ambacho kinaweza kuifunga timu yoyote kwa Tanzania na Afrika Mashariki.
Simba, wamekuwa kwa miaka minne sasa wanataabika kukifanyia marekebisho kikosi chake na kuna wakati huwaondoa wachezaji wengi na kuwaingiza wengi wapya na kukifanya kikosi kuwa kipya kila mara. Wakati Yanga wanakuwa na maingizo machache mapya na kuwa na msingi imara, Simba wao hukibomoa na kukijenga kikosi kila uchao kitu kingine chenye tofauti ya dhahiri ni aina ya wachezaji ambao Simba wamekuwa wakisajili.

Kwangu mimi Simba imekua ikitumia falsafa ya kuamini sana vijana ambayo sio mbaya, lakini naona wengi wao wanakuwa hawako sio tayari kuipa tu ubingwa bali hata kuhimili mikikimikiki ya ligi kwa ujumla wake. Simba ina mahitaji makubwa yaliyo sawasawa na Yanga na pengine kwa sasa Azam FC. Inapokuja wenzio wanahangaika kutafuta wachezaji ambao wanaonekana washindani zaidi, wewe uko na ‘chekechea’ wako inakuwa unajipunja mwenyewe.

Kitu kingine ambacho kimeinyima raha Simba ni mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi, ambapo kwa hivi karibuni wamekuwa na Milovan Cirkovic, Zdravako Logaruzic, Darren Kerr, Jackson Mayanja na sasa Joseph Omog. Hiki ni kipindi cha miaka minne wakati Yanga baada ya Ernie Brandts wakamleta Hans Van der Pluijn na mambo yanaendelea. Ukiachana na hayo yote tangu msimu umeanza Simba wameonekana kuongoza ligi tangu siku ya kwanza mpaka sasa.
Waliwafunga Ndanda 3-1, wakatoka sare ya bila kufungana na JKT Ruvu, wakawafunga Ruvu Shooting 2-1, wakawafunga Mtibwa Sugar 2-0, Azam FC 1-0 na Majimaji 4-0. Wana pointi 16 wamefungwa bao 2 na kufunga 12. Yanga wao wamewafunga African Lyon 3-0, wakatoka sare ya bila kufungana na Ndanda, wakawafunga Majimaji 3-0, Mwadui 2-0 na wakafungwa na Stand United 1-0. Wana pointi 10 wamefunga mabao 8 na kufungwa moja.
Ukiangalia huo mchanganuo hapo ni kama vile Simba wako vizuri kuliko Yanga na kuipa nafasi ya kushinda mechi hii ya watani inayochezwa leo kwenye uwanja wa taifa Dar es Salaam, lakini kiuhalisia sio kweli kabisa. Yanga wana kikosi imara kulinganisha na Simba ingawa matokeo yanaweza kwenda upande wowote. Pamoja na ubora wa Yanga lakini huwezi kudharau mtiririko wa ushindi wa Simba kwani kushinda kunakujenga na kukupa kujiamini zaidi.

Kitu kingine ambacho Yanga wanacho zaidi ya Simba kwenye mechi hii ni wachezaji wazoefu wa mpambano wa watani. Simba ina wachezaji wengi wapya kabisa kwa pambano la watani, kwa maana nyingine hawajawahi kutia mguu kwenye mechi kama hii. Wachezaji kama Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Mohamed ‘Mo’ Ibrahimu, Method Mwanjali, Malika Ndeule, Fredrick Bragnon, Laudit Mavugo, Javier Bukungu, Novat Lufungo, Hamadi Juma ambao hawajawahi kucheza kabisa mechi kama hii na wachezaji tegemezi.
Huku Yanga wao wakiwa na Juma Mahadhi, Benno Kakolanya na Obrey Chirwa pekee ndio ambao wageni kabisa wa mechi kama hii. Waliobaki wana uzoefu wa kutosha na mikikimikiki ya mechi kama hii.
Wachezaji wageni wengi wa Simba wameonesha kiwango cha kuridhisha kwenye mechi walizocheza mpaka sasa, ingawa kwenye mechi hizo ni moja tu ndiyo wamecheza na timu inayogombea ubingwa ambayo ni Azam FC. Unaweza kusema kwamba hapa ndipo hasa unapopata kuwapima kwamba wana hadhi, uwezo na kiu ya kuipa Simba ubingwa kwa kucheza na Yanga. Binafsi naipa nafasi kubwa Yanga kuibuka na ushindi kwenye mechi hii kuliko Simba ingawa Simba sio wa kubeza na matokeo yanaweza kwenda kokote.

Post a Comment

Johnny MaLcom x

{picture#https://pbs.twimg.com/media/DMZ1UrCXcAAa6Ij.jpg} Johnny malcom is the proffesional public health officer,graphic designer and amature mechanical engineer who likes blogging as much as eating. {facebook#https://www.facebook.com/Runc2} {twitter#https://twitter.com/Runcxx} {google#https://plus.google.com/u/0/113916418534820565109} {pinterest#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#https://www.instagram.com/official.seeker/?hl=en}
Powered by Blogger.