WANANCHI katika kijiji cha Kalundi wilayani Nkasi mkoani Rukwa wanadaiwa kumuua kisha kuuteketeza kwa moto mwili wa Mganga wa kienyeji, Patrick Mwandaliwa (44) wakimtuhumu kumuua mjukuu wake, Silvia Mwanakatwe mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema tukio hilo lilitokea Septemba 4 , mwaka huu, saa 2:00 usiku kijijini Kalundi wilayani Nkasi mkoani humo.
Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kyando alidai usiku huo wa tukio Mwandaliwa alikutana na mpwa wake Maria Kapele (21) dukani kijijini humo akiwa amembeba mtoto wake wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
“Mwandaliwa alimwomba mpwae (Maria) ampatie mjukuu wake huyo kisha aliondoka naye hadi nyumbani kwake, mpwae hakuwa na wasiwasi wowote kwa kuwa aliyemchukua mwanawe ni mjomba wake. Maria alihisi muda mrefu umepita tangu mjomba wake amkuchukue mtoto wake ndipo alipomtuma mtoto wa jirani yake aende kumchukua, lakini alipofika nyumbani kwa Mwandaliwa alikuta mlango wa nyumba yake umefungwa, akarudi na kumtaarifu mama yake mtoto,” alieleza.
Inadaiwa kuwa mama wa mtoto alipofika nyumbani kwa mjomba wake alimwomba ampatie mwanawe lakini alikataa kuwa hana mtoto wake ndipo Mwandaliwa alipomsukuma mpwae kumtoa nje ya nyumba yake kisha akajifungia ndani.
“Mwandaliwa alipanga magunia ya mahindi mlangoni akizuia mtu yeyote asiweze kuufungua mango ndipo mama wa mtoto alipopiga yowe akiomba msaada akiita watu. Watu walikusanyika kwenye eneo hilo la tukio, kwa kuwa walikuwa wengi waliweza kuuvunja mlango na kuingia ndani na kumkuta Mwandaliwa akiwa ameshika ndoo ya plastiki mkononi akiwa na mwili wa mtoto, tayari akiwa amekufa, akiwa amemtoboa shingoni kwa kitu chenye ncha kali," alieleza Kamanda Kyando.
Alisema ndipo wananchi wakiwa na silaha za jadi yakiwemo mawe, marungu, mapanga na vipande vya matofali walianza kumshambulia Mwandaliwa na kumsababishia kifo kisha wakauchoma mwili wake kwa moto.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mwandaliwa alikuwa ni mganga wa kienyeji, sasa inawezekana alifanya mauaji hayo kwa mambo yake ya uganga, tulikuta godoro lake likiwa limelowa damu. Inawezekana alimuua mtoto huyo hapo kabla ya kuuweka mwili wake kwenye ndoo ya plastiki,” alieleza.
Baadhi ya wakazi wa kijijini humo kwa masharti ya kutoandikwa gazetini walidai kuwa miili ya marehemu wote wawili ilifanyiwa maziko juzi kijijini humo, lakini wananchi walisusa kuuzika mwili wa Mwandaliwa huku idadi kubwa ya wakazi wa kijiji hicho walijitokeza kumzika Silvia.
Kwa mujibu wa Kyando, mwili wa Mwandaliwa ulizikwa chini ya ulinzi wa askari polisi, maziko yaliyoshuhudiwa na ndugu wa marehermu na viongozi wawili wa kijiji hicho.
Post a Comment
Post a Comment