Viongozi wengi watakusanyika leo katika mji mkuu wa Colombia, Cartagena kushuhudia kutiwa sahihi kwa kihistoria katika juhudi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimeendelea nchini humo kwa nusu karne.
Mapatano hayo na kundi la waasi la FARC ni lazima yaidhinishwe na raia katika kura ya maoni itakayopigwa October 2.
Lakini Rais Juan Manuel Santos aliambia BBC kuwa mapatano hayo yatakuwa hatua muhimu katika kuangamiza vita hivyo.
Miaka 50 ya vita nchini Colombia imeshuhudia mateso makubwa ambapo mamia ya maelfu ya watu walitekwa nyara, kuuawa au hata kutoweka wasijulikane waliko.
Wakosoaji wanasema kuwa mapatano ya sasa yanawaruhusu waasi wa FARC kukwepa haki kwa makosa waliyofanya.
Lakini rais Santos kwa upande wake anasema kuwa hayo ndiyo mapatano bora zaidi yanayoweza kufanywa kwa niaba ya Colombia.
Baadhi ya wanachama wa FARC, pamoja na maafisa wa kijeshi na polisi watafikishwa mbele ya mahakama maalumu kujibu mashtaka kwa makosa ambayo wametekeleza katika vita nchini humo.
Kundi la FARC limekubali kusalimisha bunduki zake na vitendo vyote vya uhalifu.
Ingawa hali ngumu nchini humo inafikia ukingoni lakini rais Santos anakiri kuwa kufikia amani kamili kutakuwa kugumu kama vita vyenyewe.
Alipoulizwa iwapo ana njia nyingine ya kufuata iwapo Oktoba 2, wananchi wa Colombia watakataa mpango huo, alisema kuwa njia nyingine ni moja tu ambapo wote watarejelea vita.
Post a Comment
Post a Comment