WAKATI serikali ikianza taratibu za kuhamia Dodoma, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na msimamizi wa mali za serikali kufanya uchunguzi kuona namna Sh bilioni 12.5 zilivyotumika kwenye ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambayo bado inaendelea kujengwa.

Akitoa maazimio ya kamati hiyo mara baada ya kumaliza kuihoji Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa kikao hicho, Japhet Hasunga ambaye ni Mbunge wa Vwawa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kamati inataka kujiridhisha thamani ya fedha zilizotumika katika ujenzi huo.
Katika tukio lingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Agnes Mkandya ameangua kilio wakati akihojiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kutokana na kuulizwa maswali mfululizo ya ubadhirifu wa fedha kwenye halmashauri hiyo.

Mkandya alijikuta katika wakati mgumu wakati akijibu maswali mbalimbali, yanayohusiana na ubadhirifu hali iliyofanya kuanza kulia, huku akichukua kitambaa na kujifuta machozi, hatua iliyofanya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Kilwa Mjini, Vedastus Ngombale (CUF) kumtaka kuwa mtulivu wakati akijibu maswali.

CAG na ofisi ya RC
Hasunga akieleza maazimio ya Kamati ya PAC, alisema lengo ni kujiridhisha usahihi wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa ofisi hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambayo iliungua moto miaka michache iliyopita.

“Kamati inamuomba CAG kwa kushirikiana na Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali kufanya tathmini ya kina ili kuiridhisha kamati iwapo gharama ya Sh bilioni 12.5 zilizotumika katika ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi sasa zinakidhi thamani na hali halisi ya jengo hilo lilipofikia,” alisema.
Pia kamati hiyo iliiagiza Idara ya Usimamizi Mali za Serikali, kufanya uhakiki maalumu wa mali za serikali hususan magari yanayofanya kazi, yaliyoharibika, yaliyouzwa na kuwasilisha taarifa ya uhakiki huo maalumu kwa kamati ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Mwenyekiti huyo wa Kikao, pia alimtaka Ofisa Masuhuli kusimamia kikamilifu Kitengo cha Uhasibu cha Sekretarieti ya Mkoa ili kuzingatia viwango vya kimataifa vya utayarishaji wa mahesabu katika uandaaji wa taarifa za hesabu za serikali ili kuepuka hati za ukaguzi zenye dosari.
Alisema Ofisa Masuhuli anaagizwa pia kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma na kanuni zake katika shughuli za sekretarieti, ikiwa ni pamoja na kupata vibali kwenye mamlaka husika unapofanyika uhamisho wa fedha katika vifungu mbalimbali.
Alimuagiza Ofisa Masuhuli kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhakikisha nafasi za kazi zinazokaimiwa zinajazwa mapema iwezekanavyo ili kuongeza ufanisi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma.
“Pia kuna hoja nyingi za ukaguzi bado hazijapata majibu ya kina, kamati inatoa muda wa miezi sita kwa Sekretarieti ya Mkoa kukamilisha majibu ya hoja za ukaguzi na taarifa za utekelezaji iwasilishwe kwa CAG na kwa kamati ndani ya muda huo,” alisema.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge alisema sekretarieti hiyo itafanyia kazi maagizo yote, ambayo kamati hiyo imeelekeza.
Mbunge wa Dimani, Hadith Ally Tahiri (CCM) ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alihoji sababu zilizofanya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwa na majokofu mabovu kwa muda mrefu na ubovu wa huduma zitolewazo katika Wodi ya Wagonjwa Walio katika Uangalizi Maalumu (ICU).
‘’Makao Makuu ya Nchi yanakuwa hapa Dodoma, Je, hospitali hii itaweza kuhudumia wagonjwa wote?” Alihoji.
Akijibu hoja hizo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Zainabu Chaula aliiomba kamati hiyo kusaidia hospitali hiyo iweze kupata huduma za kiwango cha kuridhisha.
DED aangua kilio akihojiwa
Katika tukio lingine lisilo la kawaida, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Agnes Mkandya jana alijikuta akiangua kilio wakati akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya LAAC, kutokana na kuulizwa maswali mfululizo ya ubadhirifu wa fedha kwenye halmashauri hiyo.
Mkandya alijikuta katika wakati mgumu wakati akijibu maswali yaliyohusu ubadhirifu, hatua iliyofanya kuanza kulia na kumlazimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ngombale, kumtaka kuwa mtulivu wakati akijibu maswali.
Tukio hilo lilitokea wakati Mkurugenzi huyo, alipoulizwa swali na Mbunge wa Viti Maalum, Leah Komanya (CCM) ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo, aliyetaka majibu kuhusu ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri ya Gairo.
Akijibu, Mkurugenzi huyo alisema amewasimamisha kazi wakuu tisa wa idara na halmashauri hiyo kutokana na ubadhirifu uliokithiri. Hata hivyo, wakati wabunge wakiendelea kusikiliza maelezo zaidi, Mkurugenzi huyo alishindwa kuendelea kujibu na badala yake kuangua kilio.
Kutokana na kitendo hicho, Mwenyekiti wa Kamati alimtaka Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri kujibu swali hilo, lakini naye aliposimama alisema wana muda mfupi tangu wakabidhiwe madaraka, hivyo inakuwa vigumu kuweza kujibu maswali yote.
Kutokana na majibu hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo alimuinua Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk John Ndunguru kujibu swali hilo, ambapo aliposimama alisema viongozi wengi ni wageni na watajitahidi kufuata maagizo watakayopewa.
Katika maelezo ya swali, Mbunge Komanya alisema Halmashauri ya Gairo imekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha kwa kutumia karatasi za nukushi (carbon slip), hivyo kuikosesha serikali mapato na kumuagiza mkurugenzi huyo kutoa majibu.
Akijibu hoja hiyo, mkurugenzi huyo alisema suala la wizi wa aina hiyo lilijitokeza ambapo walikamata mtendaji mmoja na sasa wanaendelea na kazi ya kufunga Mashine za Kielektroniki za Kukusanya Mapato (EFD’s) huku Kampuni ya Simu (TTCL) ikifanya taratibu za kuwaunganisha.
“Mimi nilikuwa natoa angalizo, nataka Mkurugenzi ajibu kama nilivyouliza, sitaki maelezo mengi,” alisema Komanya na kumfanya mkurugenzi huyo kuangua kilio na kuchukua kitambaa cha kujifuta machozi.

Post a Comment

Johnny MaLcom x

{picture#https://pbs.twimg.com/media/DMZ1UrCXcAAa6Ij.jpg} Johnny malcom is the proffesional public health officer,graphic designer and amature mechanical engineer who likes blogging as much as eating. {facebook#https://www.facebook.com/Runc2} {twitter#https://twitter.com/Runcxx} {google#https://plus.google.com/u/0/113916418534820565109} {pinterest#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#https://www.instagram.com/official.seeker/?hl=en}
Powered by Blogger.