Miili sita ya wafuasi wa upinzani, waliouawa tarehe 19 na 20 Septemba wakati wa maandamano dhidi ya Rais Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila, iliwekwa hadharani mjini Kinshasa Jumatatu hii, waandishi wa habari wa shirika la habari la AFP wamearifu.
Miili ya watu hao iliwekwa hadharani kwenye makao makuu ya chama cha UDPS, chama cha kiongozi wa upinzani wa kihistoria Etienne Tshisekedi. Wafuasi 2000 wa chama cha UDPS walikusanyika katika mahali ambapo miili hiyo sita ilikua imewekwa kwa ajili ya mazishi Jumanne wiki hii.
Familia za marehemu na wafuasi wengine wa chama cha UDPS, wengi wakitokwa na machozi, waliimba nyimbo zinazopinga serikali wakati ambapo walikua wakisafirisha miili ya watu hao kutoka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Bondeko, katika wilaya ya Limete, katikati mwa mji wa Kinshasa, ambapo miili hiyo ilihifadhiwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Chama cha UDPS, ambacho kinapanga kuzika miili ya wafuasi hao sita Jumanne katika makaburi ya Kinkole, kilomita zaidi ya 20mashariki mwa mji wa Kinshasa, kimemshtumu moja kwa moja Rais Joseph Kabila kuhusika na hali hiyo. "Wafuasi wetu waliuawa na ujinga wa Kabila, "amesema Jean-Marc Kabund, Katibu mkuu wa chama cha UDPS.
Wakati huo huo Naibu Gavana wa mji wa Kinshasa, Clement Bafiba alikumbusha wanasiasa kuheshimu hatua serikali iliyochukua hivi karibuni ya kupiga marufuku mikusanyiko yoyote ile yenye lendo la kisiasa.
Itakubukwa kwamba tarehe 19 na 20 septemba, watu wasiopungua 53, ikiwa ni pamoja na raia 49 na polisi 4 waliuawa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wakati wa maandamano yaliyoitishwa na muungano wa vyama vya upinzani wa Rassemblement.
Post a Comment
Post a Comment