Kiungo mkongwe wa timu ya taifa ya Ujerumani, Bastian Schweinsteiger, amerejea kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza cha klabu yake ya Manchester United, baada ya kuwa nje ya kikosi hicho toka ujio wa kocha Jose Mourinho.
Bastian mwenye umri wa miaka 32, amekuwa akifanya mazoezi mwenyewe pamoja na kikosi cha vijana wa chini ya umri wa miaka 23 wa klabu hiyo, toka kocha Jose Mourinho alipowasili kwenye klabu hiyo msimu huu.
Nahodha huyu wa zamani wa Ujerumani, mara ya mwisho aliichezea mashetani wekundu Manchester United mwezi Machi mwaka huu, wakati kocha Louis van Gaal alipokuwa kocha wa timu hiyo.
Mwezi Agosti mwaka huu kiungo Bastian alinukuliwa na vyombo vya habari, akisema kuwa hana tatizo lolote na kocha mpya Mourinho na kwamba Manchester United itakuwa ndio timu yake ya mwisho kucheza ikiwa atamaliza mkataba wake.
Hata hivyo licha ya kurejea kwenye mazoezi na kikosi cha kwanza cha timu hiyo, bado haijulikani ikiwa kocha Mreno Jose Mourinho, atamjumuisha miongoni mwa wachezaji wake wanaocheza ligi kuu.
Bastian aliorodheshwa kwenye kikosi cha wachezaji wa Man U watakaoshiriki ligi kuu ya Uingereza, lakini akaachwa nje ya orodha ya wachezaji wa kikosi kinachoshiriki michuano ya Europa League.
Schweinsteiger ameichezea United mara 31 toka aliposajiliwa kwa dau la paundi milioni 14.4 akitokea klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, mwezi Julai 2015.
Post a Comment
Post a Comment