MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Udalali ya Yono, wameifungia Kampuni ya Benchmark Productions na kuipa muda wa siku 14, iwe imelipa deni la kodi ya Sh bilioni 7.04, vinginevyo mali za kampuni hiyo zitauzwa kwa mnada.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Meneja Msaidizi wa Madeni wa TRA, Mkoa wa Kinondoni wa Kodi, Sylver Rutagwelera alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuidai kampuni hiyo inayomilikiwa na Rita Paulsen kwa muda mrefu bila kulipa.
TRA, wakiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono, walifika eneo la Mikocheni jijini hapo jana asubuhi ziliko ofisi za kampuni hiyo na kuwaeleza wahusika kuhusu deni hilo, na kuwataka waoneshe risiti za malipo iwapo wameshaanza kulipa deni hilo, jambo ambalo wahusika hao hawakuwa nazo.
Hata hivyo Meneja Operesheni wa Kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Evelyn alifika ofisini hapo na kuwaambia maofisa hao kuwa walishaanza mawasiliano jinsi ya kulipa deni hilo. “Zipo barua tulizokuwa tumeanza kufanya mawasiliano na TRA, kuhusu deni hili, lakini pamoja na hayo, deni lenyewe ni kubwa kuliko uwezo wa kampuni,” alisema Evelyn.
Hata hivyo Rutagwelera alisema mmiliki wa kampuni hiyo anadaiwa kodi tangu mwaka 2009 na alikuwa akitumia jina lingine kwenye kampuni hiyo na baada ya muda aliifunga na kufungua hiyo ya Benchmark ili hali deni la nyuma hajalipa.
“Mdaiwa huyo alikuwa ana kampuni aliyoipa jina lingine na tulimkumbusha kulipa kodi ya serikali tangu mwaka 2009 ila hakutekeleza na badala yake aliamua kuifunga kampuni na kufungua hii, akidhani deni limefutika”, alisema Rutagwelera.
Alisema baada ya kuona muda unasonga na deni linazidi kuongezeka bila mdaiwa kuonesha juhudi za kulipa waliamua kukabidhi mdaiwa huyo kwa Kampuni ya Yono kwa ajili ya kufuatilia deni hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela alisema wameifungia kampuni hiyo na kuanzia sasa walinzi wa Yono watalinda na baada ya muda wa siku 14, waliopewa kulipa deni hilo ukipita, watachukua hatua nyingine kisheria ya kuuza mali za kampuni hiyo kwa mnada.
Alisema deni hilo ni kubwa kwa sababu ni muda mrefu umepita kodi ya serikali haijalipwa na kuwashauri Watanzania kuacha tabia ya kulimbikiza kodi kwa sababu deni litakuwa kubwa ila likilipwa kwa wakati linaondoa usumbufu usio wa lazima.
“Yono tumepewa kazi ya kukusanya madeni ya serikali na tutaendelea kuwakamata wale wote tunaopewa kuwafuatilia lengo sio kuwaumiza ni kuhakikisha kodi ya serikali inakombolewa kwa manufaa ya nchi yetu, kwa maana tunamuunga mkono Rais John Magufuli kuhakikisha taifa letu linaendelea kwa kukusanya mapato stahiki”, alisema Kevela.
Kevela alisema kazi ya kuendelea kukusanya madeni kwa wadaiwa wengine wa serikali inaendelea na sasa wako kwenye hatua mbalimbali za ukusanyaji ikiwa ni pamoja na kuendesha mnada wa mali za wadaiwa mbalimbali ili kupata fedha za serikali.
by
Habari Leo
Habari Leo
Post a Comment
Post a Comment