Na Basili msongo.....
MAMBO vipi wangu, mwasemaje waungwana?
Poleni kwa majukumu na starehe za hapa na pale. Namshukuru Mungu kwa yote, maisha yanaendelea, leo yetu, jana historia, ya kesho fumbo, dunia ndiyo hii, maisha ndiyo haya. Walimwengu ni sisi, tuzidi kuombeana heri ili tupate tunachostahili na tufike tunapokusudia.
Mambo si mambo mdau, kufa hatufi lakini cha moto tunakiona. Kila kukicha afadhali ya jana, ukiwa na ‘heng ova’ ya ‘kilaji’ mwenzako na mning’inio wa shida. Maisha mapambano, mjini akili, kijijini kilimo tu, mtaji wa masikini nguvu zake, nguvu ya tajiri hela zake. Mtaji wa mrembo mashamsham yake.
Hakuna kulala hadi kieleweke, mchana nzi, usiku mbu, na usisahau kurukaruka kwa maharage ndiyo kuiva kwake, ukiona giza ujue kumekuchwa. Maisha ‘fweza’, ukiwanazo utaitwa mzee hata kama ni kijana. Zikikutembelea utapata kila kitu isipokuwa amani, utakwenda kila mahali isipokuwa mbinguni. Mwenye fedha si mwenzako, masikini hana wapambe.
Ukitaka kufahamu nguvu ya fedha jaribu umasikini, na ukipenda kufahamu uzuri wa kuishi kijaribu kifo. Unaishi leo, kesho si yako, ukipata fursa piga mabao kama huna akili nzuri, ukizubaa inakula kwako watu wanaenda kati.
Piga pasi fupi za ukweli, piga mashuti ya mbali, tengeneza nafasi, chezesha timu yenye njaa ya magoli, shambulia kwa kushtukiza, piga pasi za mwisho za ukweli ufanye mambo. Huu mchezo hauhitaji hasira, jilinde usifungwe bao la mapema, jiamini, waambie wapinzani wako wasipoinywa watailamba na kama hawajui kusoma kuna picha kibao uwanjani.
Maisha ni kama soka. Soka ni mchezo wa makosa, gemu likikaa vizuri unacheka tu, likikukataa utaisoma hata kimya kimya.
Maisha ni fursa, ukiipata itumie, bahati haiji mara mbili. Maisha ‘fweza’, asiyekubali hilo ana akili za ‘kichina’, maisha magumu kwako, unapojiuliza utapata wapi hela ya kula, mwenzako anajiuliza atazitumia na nani. Siku njema.
Mtafute hapa
bmsongo@gmail.com
bmsongo@gmail.com
Post a Comment
Post a Comment