Shirika la kimataifa la kukabiliana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa michezoni (Wada) limesema njia zilizotumiwa kukabiliana na matumizi ya dawa hizo michezo ya Olimpiki Rio zilijaa kasoro nyingi.
Shirika hilo limesema wanariadha wengi ambao walifaa kupimwa "hawakupatikana" wakati ambao walifaa kuchunguzwa.
Ripoti ya shirika hilo inasema katika baadhi ya siku, "wanariadha 50% waliopangiwa kupimwa" hawakupimwa.
Ripoti hiyo ya kurasa 55 imebaini kuwa kati ya wanariadha 11,470 walioshiriki, hakuna rekodi zozote za kuchunguzwa kwa wanariadha 4,125, ambao 1,913 kati yao walishiriki katika michezo 10 "ya hatari zaidi".
Ripoti hiyo pia inasema:
- sampuli 100 hazikuweza kuhusishwwa na wanariadha husika kwa sababu ya kuandikwa vibaya maelezo
- sampuli moja ilipotea lakini ikapatikana wiki mbili baada ya michezo
- shughuli ya kupima wachezaji ilikuwa ya chini sana au hata haikufanyika hata kidogo katika mashindano yaliyo na uwezekano wa juu zaidi wa wanariadha kutumia dawa za kutitimua misuli, ikiwemo unyanyuaji uzani
- hakukufanyika upimaji nje ya wakati wa mchezo katika soka, jambo ambalo Wada inasema lilishangaza
- vipimo vilivyofanyika vilipungua kwa 500 kuliko ilivyokuwa imepangwa kabla ya michezo
- bila ushirikiano kutoka kwa maafisa wa kuwapima wachezaji, ni kama mfumo wote ulifeli kabisa
- kufikia 8 Agosti, ni wanariadha 4,795 pekee waliokuwa wakiwaeleza maafisa wa Wada maeneo walipo.
Wada imelaumu Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki (IOC) kwa matatizo hayo yaliyotokea.
Post a Comment
Post a Comment